
POLISI katika eneo la Suna Magharibi, Kaunti ya Migori nchini Kenya wanamsaka mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Eunice Adhiambo mwenye umri wa makamo aliyetoweka baada ya kumdunga kisu shemeji yake na kumuua.
Eunice anadaiwa kutekeleza tukio hilo baada ya mabishano makali kuzuka baina yake na shemeji yake huyo juzi Jumanne, Disemba 24, 2019.
Kulingana na chifu wa eneo hilo Yogo Tumbo, marehemu alikuwa amemtembelea mshukiwa ambaye alimkuta akimenya mihogo (kulingana na ripoti ya Citizen TV).
Inadaiwa, jamaa alijaribu kujadiliana kuhusu jambo fulani ambalo bado halijajulikana, alimzaba kofi Eunice katika makalio yake baada ya kuhisi mshukiwa alikuwa akimpuuza.
Punde si punde, mshukiwa anadaiwa kumrukia marehemu na kumdunga mara kadhaa kifuani akitumia kisu alichokuwa nacho mkononi.
Chifu huyo alidokeza kwamba, mwenda zake alifariki papo hapo na mwili wake unahifadhiwa katika makafani ya hospitali ya Migori Level Four ukisubiri upasuaji.
Social Plugin