Ad Code

Responsive Advertisement

Mbelgiji Simba Azinasa Siri za Yanga



KOCHA mpya wa Simba, Mbelgiji, Sven Vanderboeck, amejitamba tayari ameshawajua wapinzani wake, Yanga kutokana na kuwasoma vilivyo kupitia video huku akiweka wazi kwamba Januari 4, mwakani atawamaliza mapema.

Kocha huyo amesema aliwasoma vilivyo Yanga msimu uliopita wakati akiwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’ muda ambao alikuwa akimfuatilia kiungo wake, Clatous Chama anayeichezea Simba.
Kwa mara ya kwanza, Vanderboeck aliyechukua mikoba ya Mbelgiji mwenzake Patrick Aussems, atapambana na Yanga kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara itakayopigwa Januari 4, mwakani katika Uwanja wa Taifa jijini Dar.

Kocha huyo ameliambia Gazeti la Spoti Xtra, kuwa anajua vilivyo dabi hiyo ilivyo ngumu, lakini kwake anafurahia kuicheza huku mkononi akiwa anaijua vizuri Yanga kupitia kwa kiungo wake, Chama.

“Naamini mechi hii haipo mbali kutoka sasa, watu wengi wamekuwa wakiizungumzia kutokana na aina ya ukubwa na presha inayopatikana. Kwangu ninafurahia kucheza mechi za namna hii kwa sababu zinakuwa na msisimko mkubwa na mzuri.

“Ninawafahamu vizuri wapinzani wangu kwa sababu nimewatazama mtandaoni na nimeona video zao. Wakati nilipokuwa Zambia niliangalia mechi kama hii ili kumtazama Chama, kwa hiyo ninafahamu ni aina gani ya wapinzani ambao ninaenda kukutana nao,” alimaliza kocha huyo.
Chama ambaye alijiunga na Simba msimu uliopita, tayari ameichezea Simba mechi mbili dhidi ya Yanga.
Ya kwanza iliyochezwa Septemba 30, 2018, ilimalizika kwa suluhu, kisha ile ya Februari 16, 2019. Zote hizo alikuwa kikosi cha kwanza. Wakati Simba wakizinasa siri za Yanga kwa staili hiyo, Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla, amesema: “Tunajua hii ni mechi kubwa sana kwa pande zote mbili.

Kwetu tunaendelea na maandalizi na tuko tayari kwa ajili ya mechi hii. Tunajiandaa kipekee kwa kuona tunaendelea kupata matokeo mazuri.”
Reactions