
Pengine umewahi kujiuliza au hata kushangaa kwanini wewe na jirani yako au mtu mwingine mkinunua umeme kwa gharama sawa, mnapata ujazo (units) tofauti. Hii inaweza kuwa kwa mfano wote mkinunua umeme wa TZS 5,000, yeye anapata units 41, wakati wewe unapata units 14 tu, au umeme wa TZS 10,000 yeye anapata units 75, angali wewe unapata units 28.
Ukweli ni kwamba, bei ya umeme inatofautiana kutokana na kundi la matumizi mteja alilopo mfano Matumizi Madogo ya nyumbani (D1) ambao wanatumia umeme wa majumbani ambao matumizi yao ni wastani wa KWh (units) 75 kwa mwezi wananunua umeme uniti moja kwa TZS 100 (bila kodi) endapo watazidi hapo kila unit watatozwa TZS 350 (bila kodi).
Lakini wateja wa kundi la matumizi ya kawaida (T1) hujumuisha wateja wenye matumizi ya kawaida ya umeme hususani watumiaji majumbani, biashara na viwanda vidogo, taa za barabarani na mabango. Hawa wananunua umeme unit moja TZS 292 (bila kodi), kundi hili linatumia kuazia units 75-7500 kwa mwezi. Hivyo kutofautiana kwa kundi la matumizi ndicho kinachopelekea wateja kupata units tofauti kwa kiasi kile kile cha fedha.
Hivyo endapo matumizi yako ya nyumbani hayazidi units 75 kwa mwezi, unaweza kwenda TANESCO kuomba kupunguziwa matumizi ya gharama za umeme yaani kushushwa tarifu kutoka tarifu 1 kwenda tarifu 4, ambayo itakuwezesha kupata units nyingi zaidi kwa gharama kidogo.
Social Plugin