
Papa Francis amefanya ibada ya kuziombea kulainika "nyoyo ngumu na zilizojaa ubinafsi" ili kusaidia kuondosha dhuuma duniani.
Hayo ameyasema katika hotuba yake ya Krismasi ama maarufu kama "Urbi et Orbi" ("Kwa Jiji na kwa Dunia") ambayo aliitoa moja kwa moja kutoka kwenye dirisha la Kanisa Mtakatifu Petro, Basilica jijini Vatican.
Papa alizungumzia juu ya kuta za tofauti ambazo watu wanajengewa na kuombea amani katika mataifa yaliyokumbwa na mabaa ya vita, mazingira na magonjwa.
Katika hotuba hiyo aliyalenga mataifa ya Afrika ambayo Wakristo wamekuwa wakishambuliwa.
"Nawaombea ustahamilivu na amani wale wote wanashambuliwa kutokana na imani zao, hususani wamishenari na waumini ambao wametekwa na kwa wahanga wa mashambulio ya makundi yenye msimamo mkali, hasa katika nchi za Burkina Faso, Mali, Niger na Nigeria".

Shambulio la mkesha wa Krismasi nchini Burkina Faso limesababisha vifo vya watu 35 wengi wao wakiwa wanawake. Mamia ya watu wameuawa katika nchi hiyo katika miaka michache iliyopita, wakilengwa na makundi ya kijihadi.
Papa pia ameyataja maeneo mengine ambayo yameendelea kukabiliwa na machafuko kama Syria, Lebanon, Yemeni, Iraq, Venezuela, Ukraine na Palestina.
Kwa mabadiliko mema kutokea, amesema, watu inawapasa wawe na huruma.
"Namuomba [Mungu] alainishe nyoyo zetu ambazo kwa nyakati nyingi huwa ngumu na zilizojaa ubinafsi, na atengeneze njia za mapenzi yake. Na atujaalie tabasamu lake kweye sura zetu fakiri, kwa watoto wote wa dunia: wale ambao wametelekezwa na wale ambao wanateseka kwenye magomvi," amesema.
Social Plugin