Ad Code

Responsive Advertisement

Yanga Yalia na Kupoteza Mamilioni Mbeya



Klabu ya Yanga imeeleza masikitiko yake kufuatia kuhamishwa kwa mchezo wao wa ligi dhidi ya Tanzania Prisons kutoka Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya hadi Uwanja wa Samora mjini Iringa.

Mchezo ulihamishwa kutokana na kuharibiwa kwa Uwanja wa Sokoine kufuatia tamasha la muziki lililofanyika katika uwanja huo usiku wa Disemba 25, ambapo uongozi wa Yanga umelalamikia gharama ambazo umetumia kuelekea mchezo huo.

Akizungumza baada ya kuhamishwa kwa mchezo huo, Afisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema, “tutawaandikia barua Bodi ya Ligi ili tujue kama gharama hizi atazibeba nani, tutahoji baada ya kupitia kanuni zinasemaje lakini hakukuwa na ulazima wa kulazimisha mchezo huu kuchezwa”.

“Hivi vitu sio vya kukaa kimya, sisi tumefika Iringa saa saba usiku na Tanzania Prisons wamefika saa 3 Usiku na tumetumia gharama kubwa pale zaidi ya milioni 18 ambayo ni milioni 6 ka siku na tumekaa zaidi ya siku tatu”, ameongeza Bumbuli.

Mchezo huo unatarajiwa kupigwa leo katika dimba la Samora mjini Iringa, ukiwa ni mchezo wa pili kwa Yanga katika Nyanda za Juu Kusini baada ya kucheza na Mbeya City na kutoa sare ya bila kufungana.
Reactions