STAA mpya wa Simba, Hassan Dilunga, amekiangalia kikosi cha Yanga, kisha akasema: “Waleteni hao Yanga mapema tu tumalizane nao.”
Dilunga katika kukolezea kauli yake hiyo, amejiapiza timu yake kuchukua makombe mawili ya Ligi Kuu Bara na FA huku akitoa ahadi ya kuwafunga watani wao wa jadi, Yanga na kuwatoa mikono mitupu.
Yanga na Simba zinatarajiwa kuvaana Machi 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, mchezo unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa kutokana na upinzani wa timu hizo zinapokutana.
Kauli hiyo aliitoa mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa Kombe la FA walipokutana na Stand United na kuwatoa kwenye mashindano hayo kwa kuwafunga kwa penalti 3-2 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
“Siku zote hakuna mechi nyepesi, kikubwa kinachotakiwa ni kujiandaa pekee, tunafahamu ubora na udhaifu wa Yanga, hivyo tumejiandaa kupata matokeo mazuri mara tutakapokutana nao.
“Katika msimu huu tunataka kuandika historia nyingine ndani ya Simba kwa kuhakikisha tunachukua makombe yote ikiwemo la ligi na FA.
“Pia, kuwafunga Yanga mara tutakapokutana kwani sisi kama wachezaji tumejiandaa vema katika mzunguko huu wa pili ili kuhakikisha tunafikia malengo yetu hayo,” alisema Dilunga.


0 Comments