Ad Code

Responsive Advertisement

WASIOKULA VYAKULA VYA WANGA HATARINI KUPATA MATATIZO YA UBONGO


MTAALAMU wa lishe kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Maria Samlongo, amesema wanaojinyima kula vyakula vya wanga ili kupunguza uzito wako hatarini kuathiri uwezo wa ubongo kutokana na kundi hilo la chakula kuhitajika zaidi.

Alisema vyakula vya kundi la wanga husaidia ubongo kufanya kazi kwa ufasaha na kiwango cha utendaji kazi kuongezeka zaidi.

“Mtu pia anaweza kukosa nguvu baada ya kutumia kundi moja la chakula, mfano kundi la wanga linatumiwa sana na ubongo, hivyo mtu akifanya ‘diet’ kwa kuacha kula wanga, ubongo unashindwa kufanya kazi, hauwezi, mtu atakuwa analala ubongo wake hautakuwa ‘active’ muda mrefu.

“Na sio ubongo tu, wakati mwingine unaweza kuchosha viungo vingine kama figo.

“Mtu ambaye anaamua kutumia kundi moja anachosha figo kwa sababu mwisho wa siku figo lazima ifanye kazi za kuchuja uchafu wa chakula na ukumbuke mfano protini haihitajiki kwa kiasi kikubwa, hivyo kama protini inakuwa nyingi unaweza kuchosha figo na hapo protini zinakuwa nyingi kuliko uhitaji wa mwili,” alieleza Maria.

Alisema athari ya kuongezeka uzito ni kupata magonjwa kama ya moyo, mishipa ya damu kuziba na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza.

Hata hivyo aliwashauri watu kutafuta wataalamu wa lishe ili waweze kushauriwa njia nzuri ya kupunguza uzito.

“Kumekuwa na elimu tofauti tofauti ya kupunguza uzito. Hatukatai ni kweli wanapunguza uzito kwa sababu wananyima mwili baadhi ya viini lishe, lakini hasara wanazozipata zipo za aina nyingi, zingine ni za wakati huo huo na kuna za muda mrefu.

“Kuna wengine wanajinyima kula chakula na kunywa maji siku nzima, wengine wanachukua kundi moja la chakula, mwingine juisi tu. Hatuzuii mtu kupunguza uzito, lakini punguza uzito kwa njia sahihi,” alisema Maria.

Alisema kuwa ushauri utakaotolewa na mtaalamu wa lishe utakuwa endelevu katika kuhakikisha kiwango cha uzito kubaki inavyotakiwa.

Hata hivyo, aliitaka jamii kubadilisha mfumo wa maisha ikiwemo kuacha matumizi ya vilevi na ulaji mbaya, badala yake wazingatie mlo kamili na ufanyaji mazoezi.
Reactions

Post a Comment

0 Comments